Usimdharau mteja kwa kupungukiwa fedha

Category: Kuhudumia Wateja

INAELEZWA kuwa dharau kwa mteja aliyepungukiwa fedha ya kununua bidhaa au huduma kutoka katika duka au hoteli, baa na biashara nyingine ni utovu wa nidhamu.

Mtandao wa maswali, www. ask.com unasema, nidhamu inayozungumziwa katika suala hilo ni ya biashara. Kwa mujibu wa mtandao huo, mfanyabiashara anasahau kuwa mteja mwenye kiasi kisichotosha kununua chochote katika duka lake, anaweza kuwa ubao mzuri wa matangazo ya biashara yake, ikiwa atahudumiwa kwa ukarimu.

Kutokana na maelezo ya mtandao huo, mteja wa aina hiyo, hasa kama amefika kutafuta huduna au bidhaa husika katika duka la mfanyabiashara anayemdharau, bila kuwa na lengo baya la kufanya kejeli ya bei, anaweza kusambaza habari nzuri kuhusu nidhamu aliyoiona, hasa kama ataeleweshwa ni kwa nini fedha zake hazitoshi na kutakiwa kurudi atakapopata kiasi cha kuongezea.

“Badala ya kumdharau mteja wako kwa kumwacha kwenye kaunta ya duka lako, eti kwa sababu ana fedha zisizotosha kununua bidhaa anayoitaka, ni vizuri ukampa matumaini ya kuikuta kesho ili akaongeze fedha,”mtandao huo unaeleza.

Aidha, unaonya kuwa si wakati wote wateja wanakuwa ‘wamejaa’ fedha katika pochi au mifuko yao, kwa hiyo wafanyabiashara hasa kwenye maduka makubwa na ya kati wanapaswa kujenga tabia ya kuangalia tofauti ya gharama na kiasi cha bei walichokipanga kuona endapo wanaweza kufanya liwezekanalo mteja asiondoke dukani bila bidhaa aliyoifuata.

“Ni rahisi sana, kwa wateja wanaotaka faida kubwa kupita kiasi katika bidhaa ambazo gharama zake si za juu kiasi hicho, wanaweza kupunguza kiasi cha bei walichokipanga na kuacha faida kidogo ili mteja mwenye fedha zisizotimia aipate bidhaa anayoitaka,”www.ask.com inasema. Kwa upande wa mtandao wa majibu, www.answers.com, ni afadhali kuingiza faida ya wastani katika huduma na bidhaa, kuliko kuwafukuza wateja kwa dharau, kwa sababu wamekosa kiasi cha fedha cha kutosha kununua bidhaa kwenye duka lako.

Mtandao huo nao ulikuwa na maelezo yanayofanana na ule wa maswali, kuhusu mteja aliyepungukiwa fedha kutumika kama ubao wa matangazo. Wataalamu katika mtandao huo wanasema, kwa sababu ya kufurahishwa na ukarimu wa muuza au mmiliki wa biashara, mteja aliyepungukiwa fedha anaweza kusambaza ujumbe wa sifa kwa wengine kuhusu alichokiona au alichotendewa.

“Lakini ikitokea kuwa mfanyabiashara amemfukuza mnunuzi kwa kuwa amepungukiwa fedha, habari hiyo inaweza kusambazwa kwa haraka na kuogopesha wateja wengine waliokuwa na nia ya kufuata huduma au bidhaa kwenye duka hilo,”www.answers.com inasema. Kwa ufupi, mitandao hiyo inashauri wafanyabiashara kuwachukulia wateja wote kuwa ni watu wa muhimu, wanaosababisha biashara zao ziendelee kuwa hai.

Pia, www.ask.com inashauri wafanyabiashara kutangaza bei za bidhaa na huduma zao kwa kutumia njia ambazo wateja wengi watapata taarifa kuzihusu, hivyo kuepuka kufika dukani na kuanza kushangaa bei. Pamoja na hilo, www.ask.com inaeleza kuwa ni vizuri wafanyabiashara hususan wa bidhaa wakajiwekea utaratibu wa kuzingatia utamaduni wa watu wa maeneo wanakofungua biashara kuepuka kuwakwaza na kuwakimbiza.

Unataja baadhi ya utamaduni ambao baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali wanauendekeza kuwa ni pamoja na kuomba kupunguziwa bei ya vitu wanavyokuwa wamekwenda dukani kuvinunua. Inaelezwa na wataalamu hao wa biashara kutoka katika mitandao hiyo kuwa, ni kawaida kwa watu wa maeneo fulani kuomba kushushiwa bei,hasa ya bidhaa za vitu katika maduka ya kawaida ambapo bei za bidhaa hizo hazijabandikwa mahali popote kuonesha kuwa hazipungui.

“Sasa inapotokea kuwa mfanyabiashara anataka kuendana na wateja wake waliozoea kushushiwa bei ,ni lazima apeleke dukani bidhaa zikiwa na bei iliyoongezwa kiasi ili litakapokuja ombi la kupunguza aondoe kiasi hicho kilichozidi”,mtandao huo unasema. Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema kiasi hicho ‘cha juu’ hakipaswi kuwa kikubwa wala hakistahili kuongezwa ikiwa tayari bei ya bidhaa husika imekwisha fanywa ya juu.

“Faida si lazima ipatikane yote kwa mara moja kwa kunyonya wateja. Ikiwa gharama za biashara hiyo ni za wastani, kwa kuzingatia uwezo wa wanunuzi kifedha, na kiasi cha faida kinachotakiwa, muuza au mmiliki wa duka anaweza kuamua kuweka bei za wastani pia”www. ansk.com inasema. Zaidi, mtandao huo unasema kuwa, kuna hatari kwa biashara kukosa wateja endapo mfanyabiashara ataamua kung’ang’ania bei za juu apate faida zaidi ya mara mbili.

Maelezo kutoka kwa wataalamu hao yanaonesha umuhimu wa fanyanyabiashara kujali na kuthamini wateja bila kujali wana fedha nyingi au pungufu. Siamini kama mteja anaweza kutoka alikotoka na kufika dukani kununua bidhaa anayofahamu kuwa inauzwa bei ya juu asiyoimudu. Wakati mwingine wauzaji wanafanya uamuzi wa bei bila kufanya utafiti kuona wauzaji katika maduka mengine wanatoza bidhaa au huduma husika kwa kiasi gani.

Sikatai kuwa bei katika soko huria hutegemea gharama ambazo mfanyabiashara amezitumia kununua bidhaa au kuandaa huduma anayouza, lakini, ni lazima kuwe na utaratibu wa kupanga bei si kujifanyia mambo kiholela. Mtaalamu katika www. answers.com anaweka bayana kuwa , wauzaji wengine wanapandisha bei ya bidhaa na huduma papo kwa papo kulingana na aina ya wateja wanaofika kuiulizia.

Tabia hiyo inatajwa kuwa chanzo kimojawapo cha kusababisha biashara iendeshwe kwa harasa kwa sababu wateja wanapogundua ‘ubabaishaji’ huo hukimbia. Wengi wanaofanya hivyo huwa wauzaji waliokosa uaminifu wasiohofu kuwadhihaki wateja hasa wanaposhindwa kumudu gharama wanazowatajia.

Imeandikwa na Namsembaeli Mduma Imechapishwa: 15 Desemba 2016    

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/index.php/safu/18706-tuzungumze-biashara-usimdharau-mteja-kwa-kupungukiwa-fedha

Kwa maoni wasiliana na Mwandishi kupitia Simu; 0752 779 090 au Barua pepe; namsp2000@ yahoo.com.