Faida za kufuga sungura

Category: Ufugaji Sungura

UZALISHAJI na ufugaji bora wa sungura kibiashara umewatoa kimasomaso wajasiriamali waliochangamkia na kuibuka kuwa mwarobaini wa umasikini. Ufugaji wa sungura ni shughuli ya kiuchumi inayokua kwa kasi kubwa. Sungura huzaliana ndani ya kipindi cha miezi miwili tu.

UZALISHAJI na ufugaji bora wa sungura kibiashara umewatoa kimasomaso wajasiriamali waliochangamkia na kuibuka kuwa mwarobaini wa umasikini. Ufugaji wa sungura ni shughuli ya kiuchumi inayokua kwa kasi kubwa. Sungura huzaliana ndani ya kipindi cha miezi miwili tu.

Sungura huzaliana kwa kasi watoto sita hadi 10 kwa mkupuo wa kwanza. Huzaa pia watoto 10 hadi 15 kwa mkupuo wa pili.

Mkurugenzi wa Tanzania Business Creation Company (TBCC), Elibariki Mchau anasema, ufugaji wa sungura ni rahisi. Hauhitaji eneo kubwa kwa ajili ya malisho.

Mchau anasema hayo kwenye kongamano aliloitisha kwa lengo la kutoa mafunzo juu ya faida za ufugaji wa sungura. Wakala wa Ufugaji wa Sungura Mkoa wa Dodoma, Angumbwike Ng’wavi anasema, kongamano hilo ni la pili baada ya lililofanyika Oktoba 8, mwaka jana.

“Kongamano hili limetupa faida kubwa sisi wakazi wa mkoa wa Dodoma,” anasema Ng’wavi akisisitiza wameelimisha umuhimu wa kujikita katika uchumi wa kufuga sungura kibiashara.

Mchau anasema utafiti uliowahi kufanywa na taasisi moja ya Marekani, unaonesha ili kupata nyama kilo 150 ya ng’ombe unahitaji ekari mbili za malisho lakini ili kupata kilo hizo za sungura unahitaji hatua tano kwa tano.

Nyama ya sungura ipo katika kundi la nyama nyeupe ambayo watu wengi wanashauriwa kula. Haina lehemu kama ilivyo kwa ng’ombe na mbuzi. Pia haina kemikali hatarishi.

Kutokana na ubora wa nyama yake, imepata soko kubwa la kupendwa kuliwa duniani kote, kutokana hasa na kuwa na carolies chache. Inazo 795 ikilinganishwa na kuku yenye 810, bata mzinga 1,190, kondoo 1,420, ng’ombe na nguruwe 2,015. Ufugaji wa sungura umepanda chati siyo tu kwa ajili ya nyama, bali pia, mkojo wake hutumika kama viuatilifu.

Mkojo ukizimuliwa na maji kwa kuchanganya katika uwiano wa lita tano za mkojo na 20 za maji, inatumika kama mbolea ya kunyunyizia mboga kunusuru mimea hiyo na wadudu waharibifu.

Wakati mwingine mchanganyiko huo wa maji na mkojo, unaweza kutumika kunyunyizia kwenye udongo wakati wa kuandaa ardhi kwa kilimo kwa kuchanganya na udongo kama mbolea ya majimaji.

Mbolea ya mnyama huyo ni bora kutokana na mchanganyiko wa madini yaliyomo ambayo yanafanya ifae zaidi kwa kilimo na kuongeza ubora wa udongo.

Ina fosiforasi asilimia 87, naitrojeni (2.2), potasiamu (2.30), salfa (36), kasiamu (1.26) na magnesiamu 40. Mkojo wa sungura tofauti na wanyama wengine, unatajwa kitaalamu kuwa unaweza kubadilika rangi; njano, kijani, pinki na damu ya mzee.

Hali hiyo inatokana na mwili wa sungura kutokuwa na asidi, kazi ambayo inafanywa vizuri na ini pamoja na kongosho kuchuja na kutoka nje.

Mchau anaelezea pia kichwa cha mnyama huyo kuwa ni dawa muhimu kwao. Kikitengenezwa supu, inasaidia kuongeza nguvu za kiume.

Sungura wana soko la uhakika na kubwa nje ya nchi, ambalo pia linawezekana kuwapo Tanzania kutokana na uhakika wa kampuni yake kuwa mnunuzi mkuu wa nyama yake kutoka kwa wafugaji.

Mfugaji anatakiwa kujikita katika kufuga sungura bora ambapo wazazi wake sita ambao ni dume mmoja na majike sita anapata kutoka kampuni hiyo kwa Sh 85,000 kila mmoja.

TBCC inatoa mkataba kwa mfugaji ili kuwa na uhakika wa soko la sungura wake. Sungura waliozalishwa watanunuliwa wakiwa hai kila wanapofika umri wa miezi minne hadi mitano.

Katika kurahisisha fursa hiyo, kampuni inatoa mafunzo kwa wafugaji na pia huduma ya utengenezi wa mabanda yake ya kufugia sungura wazazi na watoto wakizaliwa. Sungura akifugwa vizuri anakuwa na uzito wa kilo tatu hadi tano, na kampuni hiyo inanunua kwa Sh 8,000 na kuuzwa kwa masoko mbalimbali likiwamo la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Mchau anasema, ili kufikia uzito mkubwa, lazima atunzwe na alishwe vizuri chakula bora maalumu chenye virutubisho. Hulishwa majani makavu na mabichi, hupewa madini, vitamini, maji safi na salama ambayo hayana chumvi au kemikali hatarishi.

Akilishwa vizuri, sungura jike anaweza kuzaa mara sita ambapo kila uzao anaweza kuzaa watoto sita hadi 10 na mara sita ni sawa na kuzaa sungura 36 hadi 60.

Hivyo kwa jozi moja ya sungura dume mmoja na majike sita, tegemea kupata sungura 216 hadi 360 kwa mwaka, pasipo kuongeza jozi nyingine ya wazazi.

Sungura hubeba mimba kwa siku kati ya 26 hadi 31, na anatumia saa nne hadi sita kuzaa watoto alionao tumboni kama ni 10 hadi 15, ambao huzaa mmoja baada ya mwingine.

Kama wanyama wengine, baada ya kuzaa huwalamba na watoto huanza maisha wakitafuta matiti ya mama wanyonye. Sungura huzaliwa akiwa hawaoni na hawana manyoya bali huanza kutoka siku ya kwanza hadi ya tano.

Siku ya saba, watoto wanaanza kufungua macho na ya 10 wanakuwa na macho maangavu. Baada ya siku 14 tangu kuzaliwa kwao, na tangu hapo watatoka kwenye kikasha na kula chochote anachokula mama yao.

 Chanzo (HABARILEO) : http://www.habarileo.co.tz/index.php/makala/20325-faida-za-kufuga-sungura

Mwandishi: MAGNUS MAHENGE , kuchapishwa 25 Jan 2017