Vanila ni zao lenye soko kubwa

Category: Kilimo cha Vanila

Mbali na Tanzania, vanilla pia hulimwa katika nchi za Madagascar, Mexico, Uganda, Visiwa vya Comoro na katika visiwa vya Re Union. Hapa nchini zao hili hulimwa zaidi mkoani Kagera lakini sasa limeanza kusambazwa katika mikoa mingine kama vile Morogoro na Kilimanjaro. Hatua hiyo ya kusambaa kwa vanilla imeelezwa kwamba ni kutokana na juhudi za Wizara ya Kilimo na Ushirika.

Zao la vanila hukua zaidi katika maeneo yenye hali ya joto, mvua na jua kwa pamoja; hali ya hewa ya joto kuanzia nyuzi 21 C hadi 30 C. Kiasi cha mvua kinachofaa zaidi ni kuanzia mililita 1,250 hadi mililita 1,500 kwa mwaka na unyevunyevu ni muhimu pia. Kwa vile mmea wa vanilla hukua na kurefuka na kuwa mzito mkulima anahitaji kuwa na mhimili.

 Katika eneo ambalo hakuna mibuni na migomba inashauriwa mkulima apande mibuni kaburi (Jatropha) yenye kawaida ya kuota katika maeneo mengi yenye hali ya hewa tofauti. Katika hali hiyo, mkulima anashauriwa kupanda mbegu za Jatropha mbili katika umbali wa sm 60 – 70 kila upande ili kutoa mhimili kila upande.

  Kwa Mkoa wa Kagera mara nyingi wakulima hupanda Vanilla kipindi cha kipupwe, kuanzia Januari hadi Machi 15, Masika kuanzia Machi 15 hai Juni 15, kiangazi ni Juni 15 hadi Septemba 15 huku vuli ikianza mwezi huo na kuisha Desemba 31. Udongo ulio na rutuba nyingi na unaopitisha maji huwezesha vanilla kukua haraka.

 Udongo tifutifu ni mzuri kwa kilimo hiki ukilinganisha na udongo wa mfinyanzi ambao hufanya Vanilla kuota kwa shida hata kudumaa. Inashauriwa pia mkulima kuepukana kupanda zao hili katika udongo wa kichanga ambako anaweza asipate matokeo mazuri. Katika maelezo ya hapo juu, Vanila huhitaji kivuli kwa kuwa haistawi kwenye uwazi na pia inahitaji mti wa kutambaa juu yake, yaani mhimili.

  Wakati wa upandaji vanilla kivuli kinachofikia asilimia 50 kinahitajika na hupungua hadi kubaki theluthi moja wakati wa kuchavusha maua. Mwanga mkali husababisha majani kubabuka. Kama kivuli ni kingi pia mimea hukua taratibu sana.

  Mbali na mibuni aina ya miti mwingine unaofaa kwa kilimo cha Vanilla kama mhimili pamoja na kutoa kivuli ni mti aina ya Glyricidi sepium (Gilirisidia) Vanilla ni kiungo ambacho kinatumika katika matumizi mbalimbali hususani katika mabarafu, biskuti za Chocoleti pamoja na vinywaji kama soda na chai. Pia hutumika katika michanganyiko ya vitu vitamu kama sukari, peremende na maandazi.

Kwa watu ambao ni wajasiriamali na wabunifu katika matumizi ya mimea mbalimbali, hutumia zao hilo kwa ajili ya kutengenezea manukato, sabuni, mafuta laini na vipodozi. Mkoani Kagera, Vanilla ni zao la kibiashara ambalo limewasaidia wakulima wengi kujiongezea kipato. Historia ya zao hili mkoani Kagera inaanzia miaka ya 1940.

  Lakini ni miaka ya hivi karibuni ndipo vanilla imepata kutambulika na kulimwa kibiashara. Miaka ya 90, wakati bei ya zao hili ilipopanda ndipo watu wengi walihamasika kujiunga na kilimo cha zao hili. Hata hivyo inaeleza kwamba uzalishaji wa vanilla mkoani Kagera ulisuka baada ya Madagascar kufanya uzalishaji mkubwa wa zao hilo.

 Madagascar iliharibu soko la vanila, si kwa Tanzania pekee bali hata nchi zingine kiasi cha kuwepo kwa taarifa za baadhi ya wakulima kung’oa miche na kuhamia kwenye kilimo cha mazao mengine. Katika kusimamia zao hilo mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Kampuni ya Maruk Vanilla Farming and Processing (MVFP) LTD, Murshid Hassan, anasema kwa muda mrefu wamejitahidi kuwa watetezi na mabalozi wa vanila.

 Anasema kwa muda mrefu walikuwa ni wanunuzi pekee wa zao hili mkoani Kagera hadi miaka ya hivi karibuni na kwamba wadau wao wa maendeleo pamoja na serikali mchango wao bado haujatosheleza kusaidia kukua kwa zao hilo. Pia anasema ziko changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ndogo kilimo cha zao la vanila ikiwemo uzalishaji mdogo na usiokidhi viwango vya soko la kimataifa.

 Murshid anasema kampuni yao imekuwa ikikabiliana na changamoto hiyo na wamekuwa wakijitahidi kuonesha jinsi uzalishaji ulivyo na kwamba changamoto ya namna hiyo inaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. “Imani yetu imejengwa juu ya uzoefu tuliokusanya kama wakulima, kisha wanunuzi na wasindikaji. Tukiwa kama wakulima tunatambua kuwa miche mingi kwenye mashamba ya wakulima ni mizee na haipati matunzo mazuri,” anasema.

Hassan na anaongeza: “Pia tunatambua kuwa baadhi ya wakulima wameng’oa miche mizuri na kuachana na zao hili kutokana na mifumo isiyo rafiki katika manunuzi. Mathalani mkulima kumkopesha mnunuzi kwa mwaka mzima tena bila riba.” Anasema kuwa MVFP Ltd wamekuwa katika Programu endelevu ya usambazaji wa miche mipya kwa wakulima wa vijijini.

  Anafafanua kwamba mpaka sasa wamewafikia zaidi ya wakulima 400 na pia wameunganisha wakulima wapya na wazoefu ili kujifunza kwa vitendo; kuhakikisha wakulima wanajenga mapenzi ya kudumu na hawavunjwi moyo tena na mfumo wa manunuzi.

 Anasema tofauti na wanunuzi wengine, MVFP Ltd imekuwa na sera ya malipo ya papo kwa papo, sera ambayo imetekelezwa kikamilifu mfululizo bila kuvunjwa toka walipoanza kujishughulisha na ununuzi wa zao hilo takribani miaka mitatu iliyopita.

  “Mwaka 2011 MVFP Ltd ilishiriki maonesho ya BioFasch Ujerumani. Mwakilishi wetu alikutana na wanunuzi na wauzaji mbalimbali wa viungo vya chakula (spices). Miongoni mwao ni magwiji wa uuzaji wa vanila kama Nielsen Massey ambao walivutiwa na sampuli za vanilla yetu na kisha waliamua kuingia mkataba wa manunuzi na kampuni yetu,’’ anafafanua.

  Anasema wanunuzi hao waliwataka kwa miaka mitatu mfululizo kupeleka tani 15-20 za vanila kavu ya dalaja la I & II sawa na tani 100 za mapodo; uzalishaji ambao haujapata kufikiwa miaka ya karibuni mkoani humo. Vilevile anasema kampuni yo imekuwa ikiendelea kujitangaza katika maonysho mbalimbali na kwenye mitandao ya vyama vya kisekta nchini na Kanda ya Afrika na duniani kote.

 ‘’Kupitia kwenye mitandao ya intaneti, tumekuwa tukipata orders (maombi ya kupelekwa bidhaa) zilizothibitika kuwa za kweli kutoka kila pembe ya dunia kuanzia Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani, Pakistan, Afrika Kusini hadi Marekani.’’

  Kwa mujibu wa Murshid, changamoto inayowafanya washindwe kunufaika na maombi hayo ni uzalishaji duni na kwamba tatizo siyo soko. Kutokana na mtazamo huo, wadau wa kukuza zao la vanila wametakiwa kushirikiana kutatua changamoto ya uzalishaji.

 Chanzo cha Habari (http://www.habarileo.co.tz/index.php/makala/38752-vanila-zao-lenye-soko-kubwa-uzalishaji-mdogo), 03 June 2015 By Francisca Emmanuel